Sunday, April 3, 2011

Loliondo Kwarindima....

WASIRA, MKONO NAO WATUA KWA BABU KUPATA KIKOMBE
 Neville Meena na Mussa Juma, Samunge
 SAFARI za vigogo wa Serikali kwenda kijijini Samunge, Loliondo kwa Mchungaji Ambilikile Mwasapila kunywa dawa ya kutibu magonjwa sugu, zimeanza tena baada ya kusimama kwa siku kadhaa kutokana na kupungua kwa msongamano mkubwa wa magari uliokuwapo.Kupungua kwa foleni hiyo yapata siku mbili zilizopita, kumetoa fursa ya kuanza kwa utaratibu mpya wa kuruhusu magari machache yanayokwenda Samunge na jana safari za vigogo zilianza tena.

Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira na Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Nimrod Mkono jana waliingia katika orodha ya vigogo ambao wamefika Samunge kwa Mchungaji Mwasapila kupata kikombe cha dawa ambayo inadaiwa kuwa tiba ya magonjwa sugu.

Machi 27, mwaka huu Serikali ilisitisha safari za magari kwenda Samunge sambamba na kuwataka vigogo waliokuwa wakitumia ndege na helikopta kutokwenda kijijini hapo hadi foleni ya magari iliyokuwapo itakapopungua.

Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawa Lali aliliambia Mwananchi kuwa walikuwa wamewaomba mawaziri na viongozi wengine wa ngazi za juu kutopanga safari za kwenda Loliondo kwa Babu bila kuwasiliana na uongozi wa Serikali wa wilaya, lengo likiwa ni kudhibiti msongamano mkubwa uliokuwapo.

Msongamano wa magari ulikuwa ukisababisha mateso kwa watu waliokuwa wakienda kupata dawa na baadhi ya wagonjwa wafariki dunia wakiwa kwenye foleni hiyo na wengine iliwachukua kati ya siku saba hadi kumi na moja kufika kwa Mchungaji Mwasapila kupata dawa.

Wassira na Mkono wote wakiwa wabunge kutoka mkoani Mara, walifika Samunge majira ya saa nane mchana wakiwa kwenye gari la pamoja na kwenda moja kwa moja kwenye kibanda cha kutolea dawa na kila mmoja alipata kikombe cha dawa hiyo.

Akizungumza baada ya kupata dawa hiyo, Wassira alisema tiba inayotolewa na Mchungaji Mwasapila ni ya iana yake, si Tanzania tu, bali dunia nzima.

"Mimi nasema hapa ni mahali pa aina yake, katika nchi yetu na hata kwingineko duniani sijawahi kuona kiasi kikubwa cha watu wakikimbilia sehemu moja kupata tiba kama hapa," alisema Wassira na kuongeza:

"Wapo mamia ya Watanzania hapa na nimeambiwa hapa watu walikuwepo kwa maelfu. Lakini pia wapo watu wanaotoka nje ya nchi kuja hapa si jambo la kawaida... Nasema hili ni tukio la aina yake, si la kawaida tena si Tanzania tu, bali hata duniani kote," alisema.

Alisema mbali na majukumu ya kikazi yaliyomfanya kufika Samunge, lakini pia ametumia fursa hiyo kunywa dawa kama ambavyo mamia kwa maelfu ya Watanzania wamekuwa wakifanya.

"Watu wote wanakunywa dawa, kwa nini mimi nisinywe? Nimepata kikombe cha dawa, hilo siyo siri ijapokuwa muhimu ni mambo mawili makubwa ambayo yamenisababisha kufika hapa," alisema Wassira.

Alisema akiwa Waziri mwenye dhamana ya uhusiano wa jamii alilazimika kufika Samunge kuona jinsi watu wanavyoweza kuhimili mazingira hayo ambayo ghafla yamekuwa na watu wengi kwa wakati mmoja na bila kutarajia.

Wassira na waliokwama Bunda
Wassira ambaye pia ni Mbunge wa Bunda (CCM) alisema kuna idadi kubwa ya watu walikwama katika Mji wa Bunda, mkoani Mara kutokana na idadi ndogo ya magari yanayoruhusiwa kupita katika kizuizi.

"Pale Bunda ni njia kuu ya magari kutoka Tabora, Mwanza, Kagera, Shinyanga na baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Mara. Nina taarifa kwamba kuna magari zaidi ya 300 pale yamekwama kutokana na kuzuiwa yakisubiri ruhusa ya kuja huku," alisema.

Alisema kutokana na hali hiyo, leo atawasiliana Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi ili kuomba magari yanayopita Bunda kuongezwa kutoka 30 yanayoruhusiwa hivi sasa.

"Hili nitalifanyia kazi maana unaweza kudhibiti hali ikawa nzuri hapa lakini ukahamishia tatizo lilelile na msongamano sehemu nyingine. Sasa nikiwa Mbunge wa Bunda lazima nilifanyie kazi suala hili."

Mkono amwaga msaada Samunge
Kwa upande wake, Mkono aliahidi kutoa msaada wa kujenga sehemu ambayo Mchungaji Mwasapila anatolea dawa
sambamba na kuweka maturubai kwa ajili ya kuwawezesha watu wanaofika kunywa dawa kupata sehemu ya kupumzikia kwa muda.

"Nitaangalia kesho (leo) au keshokutwa (kesho) mimi mwenyewe au nitamtuma binti yangu aje hapa kuona jinsi tunavyoweza kuyaweka mazingira haya katika hali ya kutoa huduma bora zaidi," alisema Mkono na kuongeza:

"Haya yaliyopo sasa si maturubai bora yanayokidhi huduma inayotolewa mahali hapa na mchungaji".

Mchungaji awapasha wanaopinga
Jana Mchungaji Mwasapila aliwageuka wanaopinga huduma ya tiba anayoitoa kwa kusema kwamba hawapaswi kumlaumu yeye bali wamuulize Mungu aliyemtuma.

Akiwahutubia waumini waliofika kwenye ibada ya Jumapili iliyofanyika KKKT - Usharika wa Sonjo, Mchungaji Mwasapila alisema Mungu amekuwa akiwatumia watu ambalimbali kutenda miujiza lakini tatizo kubwa wamekuwa wakijitukuza wao na majina yao badala ya kumtukuza Mungu.

"Tatizo ni kwamba badala ya kumtukuza Mungu wanayemtumikia, baadhi yao wamekuwa wakitukuza majina yao, sasa Mungu ameamua kuweka neno lake kwenye mti," alisema na kushangiliwa na waumini waliofurika katika kanisa hilo.

Kampuni za simu zapigana vikumbo Samunge
Kampuni za simu za Vodacom na Airtel zimeanza kupigana vikumbo katika Kijiji cha Samunge zikiwania kuweka minara baada ya kubaini uwepo wa biashara kubwa ya mawasiliano kwa sasa kutokana na maelfu ya watu kutoka ndani na nje ya nchi kufurika katika kijiji hicho.

Timu ya waandishi wa Gazeti la Mwananchi, ambayo imeweka kambi katika kijiji hicho, jana ilishuhudia hekaheka kubwa za maofisa wa kampuni hizo za simu wakisimamia ujenzi wa maeneo ya minara  na wengine wakitafuta maeneo mengine ya kuweka minara ya mawasiliano.
Mchakato huo wa kuweka mawasiliano katika eneo hilo umetokana na maombi ya muda mrefu ya wananchi wanaofika kupata tiba Samunge ambao wamekuwa wakipotea na kushindwa kuonana na wenzao hivyo kukwama kurejea makwao.

Diwani wa Kata ya Samunge, Jackson Sandea alisema jana kuwa wamefikia makubaliano na Kampuni ya Airtel kufunga mnara wao katika eneo la Mlima Mwegaro.

“Kama unavyoona mnara unajengwa na siku si nyingi utakuwa tayari na hivyo kurahisisha mawasiliano katika eneo hili la Samunge na vijiji vyote vya jirani,” alisema Sandea.

Akizungumzia tatizo la mawasiliano katika Kijiji cha Samunge na barabara nzima kutoka eneo la Kigongoni wilayani Monduli hadi kufika Loliondo, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro alisema malumbano ya mipaka ya vijiji pia yalichangia kuchelewa huduma hiyo.

Lali alisema Kampuni ya Airtel mwaka mmoja uliopita ilitaka kuweka mnara eneo la Mwegaro lakini kuliibuka mgogoro wa mipaka baina ya Kijiji cha Samunge na Mgongo Mageri.

“Zile vurugu zilisababisha kusitishwa kwa mpango huo kwani kila kijiji kilikuwa kikitaka umiliki wa eneo la Mnara,” alisema Lali.

Hata hivyo, alisema kutokana na huduma ya Mchungaji Mwasapila, sasa wamelazimika kuomba upya kuwekwa huduma za mawasiliano katika kijiji hicho ili kuondoa adha ya wagonjwa kukosa mawasiliano.

No comments:

Post a Comment